Tuesday, November 24, 2015

hapa kazi tu na magufuri

'Elimu bure' isizalishe wahitimu wasio na maarifa

24th November 2015
Chapa
Rais John Magufuli.
Rais John Magufuli ameahidi kuanzia Januari, 2016 serikali ihakikishe inatoa  elimu bure kwa wanafunzi wote shule za msingi na sekondari za sekondari.
 
Watoto wanahudhuria shuleni, lakini swali kubwa la kujiuliza ‘je, wanajifunza?’. 
 
Taarifa za utafiti kadhaa, zimeonesha kuwa watoto wengi wanafika hadi Darasa la saba lakini hawana maarifa na Stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK). Stadi hizi ni muhimu sana kwa ajili ya ngazi za juu za elimu au kupata maarifa mengine yoyote katika jamii.
 
Kwa mfano kulingana na malengo ya mtaala wa elimu ya msingi ya Tanzania, watoto wa darasa la tatu na kuendelea wanapaswa kuwa na Stadi za Ngazi ya Darasa la Pili za Kusoma na Kuhesabu. Hata hivyo, Tathmini za Uwezo za Miaka kadhaa (2011, 2012, 2014 na 2015) zimeonesha kuwa, watoto wengi wa darasa la tatu na kuendelea, wamekuwa na kiwango hafifu cha stadi za KKK. Zaidi sana kiwango duni sana kinajitokeza kwa somo la Kiingereza.
 
Iwapo watoto wetu wanakamilisha elimu ya msingi bila kuwa na stadi za msingi za KKK, ambazo ni muhimu sana kuwawezesha kumudu masomo ya ngazi za juu, tunapaswa kuwa na mashaka sana juu ya hatima ya watoto wetu. 
 
Mathalani tathmini ya Uwezo hapo awali, unajenga hoja yangu kuwa kupiga jaramba juu ya ‘elimu ya bure’ bila kuwa na mipango mahsusi na rasilimali za kutosha kuwekeza kwa umakini kunaweza kusababisha kuwa na kizazi cha wahitimu ambao hawana maarifa. 
 
Hii ikiwa na maana kuwa wamepitia elimu ya msingi, lakini mazingira katika shule zetu hayakuwawezesha kupata stadi na maarifa stahiki kwa ngazi husika ya elimu.
 
Mzazi umepata kujiuliza, ‘kwa nini mtoto wangu anaenda shule, lakini hakuna stadi wala maarifa anayojifunza?’
 
Kuna sababu kadhaa zinazosababisha watoto wetu wasipate stadi na maarifa tunayotarajia wapate huko shuleni. 
Baadhi ya sababu zinazopelekea watoto kupata stadi na maarifa hafifu:
 
Kwanza, mahudhurio hafifu au utoro:kuhudhuria shule ni moja ya sababu muhimu sana kumwezesha mtoto kujifunza vizuri. Mahudhurio hafifu au utoro wa muda mrefu husababisha matokeo hafifu ya kujifunza. Mfano, wakati wa Tathmini ya Uwezo ya mwaka 2013, ilidhihirika kuwa kiwango cha mahudhurio kwa wanafunzi wa darasa la saba katika shule zilizofanyiwa Tathmini kilikuwa chini ya asilimia 40 kwa wanafunzi wa kike na wa kiume.
 
Tofauti ya mahudhurio shuleni kimkoa pia ilidhihirika. Mkoa wa Kilimanjaro ulionyesha mahudhurio ya juu kwa asilimia 81, wakati mkoa wa Kigoma ulikuwa na kiwango cha chini kwa asilimia 56. Ukifuatilia matokeo ya mitihani katika mikoa hii yanaendana sawia na kiwango cha mahudhurio.
 
Wataalmu wa elimu wanaafikiana kuwa, wanafunzi ambao hawana mahudhurio mazuri shukeni hukosa maarifa stahiki, na wengi huishia kuacha shule mapema na wanaweza kukosa ajira kwa muda mrefu, na kuingia katika lindi la umaskini.
 
Watendaji katika sekta ya elimu kwa ushirikiano na wadau wa elimu ikiwemo wazazi, wanaweza kukabiliana na changamoto hii ya utoro na mahudhurio hafifu ili kuongeza kiwango cha mahudhurio shuleni, na hatimaye wanafunzi kupata stadi na maarifa stahiki.
 
Mahudhurio au utoro wa walimu husababisha wanafunzi wakose muda wa kupata stadi na maarifa stahiki. Hii huathiri sana matokeo ya baadaye ya wanafunzi husika. Mfano matokeo ya Tathmini ya Uwezo ya mwaka 2015, yalionesha kuwa, wastani wa taifa wa mahudhurio ya walimu ni asilimia 75. 
 
Kwa maneno mengine, Mwalimu mmoja kati ya walimu wanne hakuhudhuria shuleni siku ambayo Tathmini ya Uwezo ilifanywa. 
 
Takwimu nyingine zinaonesha kuwa, walimu watatu kati ya walimu 10 hawakuwepo shuleni katika mikoa ya Pwani na Mwanza; halikadhalika chini ya walimu wawili kati ya 10 hawakuwepo shuleni katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Kagera, wakati Tathmini ya Uwezo ilipokuwa ikifanyika.
 
Pili, uwiano kati ya idadi ya walimu na wanafunzi: kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, wanafunzi wengi sana wameandikishwa katika shule za msingi, wakati idadi ya walimu walioajiriwa ni wachache sana.
 
Hali hii imesababisha kuongezeka kwa mzigo wa kufundisha kwa walimu. Kuna shule ambazo Mwalimu anafundisha darasa la wanafunzi hadi 120! Hali hii huweza kusababisha Mwalimu akakosa muda wa kutoa msaada wa moja kwa moja kwa kila mwanafunzi anayehitaji msaada wa ziada katika kujifunza. 
 
Tatu, mazingira hafifu ya shule.Kukosekana kwa vitendea kazi na huduma muhimu shuleni kama vile madarasa, vitabu, vyoo, maktaba, na huduma kama vile maji salama ya kunywa, chakula na huduma za afya, ni mambo muhimu sana kwa mazingira ya shule. 
 
Tathmini ya Uwezo ya mwaka 2015 inaonesha kuwa, shule nyingi zina huduma chache au hazina kabisa huduma hizi, hivyo kusababisha mazingira ya shule yasiwe rafiki kwa kujifunza. 
 
Nne, uwiano wa chumba cha darasa na wanafunzi: Sera ya Elimu inaelekeza kuwa, uwiano kati ya darasa na idadi ya wanfunzi ni chumba kimoja kitumiwe na wanafunzi 45 (1:45) kwa shule za msingi, wakati kwa shule za awali chumba kimoja kinatakiwa kitumike kwa wanafunzi 25. 
 
Hata hivyo, katika shule nyingi uwiano huu huwa mkubwa na watoto husongamana katika chumba cha darasa. Mfano, wakati wa Tathmini ya Uwezo ya 2015, katika Shule ya Msingi ya Mshikamano, ilionesha kuwa kuna watoto 126 wa shule ya awali, ambao wamesongamana katika madarasa mawili. 
 
Hapa ilitakiwa kuwe na vyumba vitano vya shule ya awali  kutosheleza mahitaji ya Sera ya Elimu, ili watoto wajifunze vizuri. 
 
Tutambue kuwa msongamano madarasani huathiri kujifunza kwa watoto wetu hasa wa madarasa ya awali.
 
Tano, baadhi ya walimu kukosa ari ya kufundisha: katika nchi hii. Walimu wamekuwa ‘mashujaa waliosahaulika’. 
 
Tumesahau kuwa wao tumewakabidhi jukumu la kuumba akili za watoto wetu ili kutimiza malengo ya Taifa katika kupata rasilimali watu ya kuwa viongozi, wataalamu na wananchi waliostaarabika kwa maendeleo ya Taifa letu. 
 
Sita, mafunzo kwa walimu. Walimu ambao hawapati mafunzo kazini mara kwa mara hupungukiwa maarifa. Kwa hoja hii, ile dhana ya ‘Elimu ya Msingi kwa Wote’ (kwa kiingereza ni Universal Primary Education (UPE), hii ‘UPE’ ilitafsiriwa kwa kejeli kama ‘Ualimu Pasipo Elimu’
 
Mipango na usimamizi mbovu wa sekta ya elimu: huenda tatizo kubwa isiwe ni udahili wa watoto wengi shuleni, lakini usimamizi mbovu wa sekta ya elimu kuanzia Wizara ya elimu hadi ngazi ya taasisi za elimu ndiyo shida kubwa sana, inayopelekea matokeo mabaya tunayoyaona sasa. 
 
Hivi shule ya msingi inawezaje ikaendeshwa kwa mafanikio iwapo ruzuku ya elimu inakawia kufika, na katika kiwango kidogo? Iweje kiwango cha elimu kikue wakati walimu wanalipwa mshahara mdogo, lakini zaidi hata huo mshahara mdogo hukawia sana kulipwa? 
 
Shule zitakuwaje na viwango vya juu, wakati wakaguzi hawajawahi kufika zaidi ya miaka mitano? Ni vipi viwango vya ufundishaji na ufaulu vifikiwe wakati shule hazina vifaa muhimu? Ni vipi viwango vya ufundishaji na ufaulu viboreshwe  wakatiwakuu wa shule wanateuliwa bila kuzingatia ujuzi na maarifa yao, na hawapati mafunzo ya uongozi?
 
Ni pale tu tutakapoweka juhudi katika kuimarisha mipango na usimamizi wa sekta ya elimu ndiyo tutaongeza viwango vya ubora wa elimu yetu.
 
Kwa kipindi kirefu tumeweka lengo katika kufaulu mitihani kuliko kuhakikisha watoto wetu wanapata ujuzi na maarifa. 
 
Hivyo, walimu huwalazimisha watoto wetu kusoma kwa kukariri ili wafaulu mitihani, na hawafundishwi kuwa na uwezo wa kutafakari na kuhoji mambo. Kwa sasa mwanafunzi anayepata ‘A’ au Daraja la kwanza, haimaniishi ni mwenye ujuzi wala maarifa, hutegemea kama alichokariri tu kilitokea katika mtihani. Kuna wakati nadhani mitihani haiwezi kupima kiwango cha maarifa ya mtu.
 
Kukosekana kwa rasilimali za kutosha: kiasi kikubwa cha bajeti yetu hutegemea wafadhili wa nje. Hivyo, wakitetereka tu kidogo katika kutoa msaada basi na programu zetu za elimu nazo zinatetereka. Kuna umuhimu kukuza vyanzo vya ndani vya mapato ili kusaidia elimu yetu. 
 
Ili kuweka mambo sawa tunahitaji kuchambua elimu yetu ya sasa, kuwe na utashi na dhamira ya dhati ya kisiasa, mipango bora, uwekezaji wa uhakika, mafunzo bora ya walimu, kuhuishwa mitaala na mfumo bora wa udhibiti wa ubora

No comments:

Post a Comment