WAKATI wabunge wateule wakianza kujisajili leo tayari kwa vikao muhimu vya kwanza vya Bunge la 11 wiki ijayo ikiwamo kumchagua Spika na Waziri Mkuu, Serikali ya Mkoa wa Dodoma imesema imejipanga vyema kuupokea ugeni huo na kuuhudumia huku ikisisitiza amri iliyowekwa ya kuzuia mikutano ya hadhara na maandamano iko palepale.
Wabunge wametakiwa kujisajili kuanzia leo mjini hapa hadi keshokutwa Jumapili, wakati Jumatatu ijayo itakuwa ni siku ya kupeana maelekezo, kutembelea Ukumbi wa Bunge na mikutano ya kamati za vyama vya siasa.
Kwa mujibu wa ratiba ya Ofisi ya Bunge iliyotolewa wiki iliyopita, Jumanne ya Novemba 17, itakuwa siku ya kuanza kwa kikao cha kwanza kwa kusomwa Tangazo la Rais la Kuitisha Bunge, ikifuatiwa na uchaguzi wa Spika, Kiapo cha Uaminifu na Kiapo cha Spika na kisha Kiapo cha Uaminifu kwa wabunge wote.
Wabunge wataendelea kuapa hadi Alhamisi asubuhi, na kisha jioni watathibitisha uteuzi wa Waziri Mkuu, uchaguzi wa Naibu Spika na kisha ataapishwa. Ijumaa, Rais John Magufuli atalihutubia Bunge.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kutokana na kuanza upya kwa pilikapilika za kisiasa hususani vikao vya Bunge, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Galawa alisema amri hiyo ya kuzuia mikutano ya hadhara na maandamano ya vyama vya siasa bado inaendelea ili kuweka utulivu muda wote wa vikao vya Bunge.
“Amri ya kuzuia mikutano wakati wa Bunge iliwekwa na Kamati nzima ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wetu ili kuwezesha Bunge kutekeleza majukumu yake bila kubughudhiwa na watu au vikundi fulani vyenye nia mbaya ya kuvuruga usalama wetu,” alifafanua Galawa.
Wabunge na wageni mbalimbali wameshaanza kuwasili mjini Dodoma na Galawa aliweka wazi kuwa mkoa umejipanga vizuri kuwapokea na kuwahudumia wabunge na wageni wote watakaoingia. Alisema mkoa una uzoefu wa kuwapokea wageni wengi kwa mara moja kwa muda mrefu hivyo kila atakayekuja asiwe na wasiwasi wa mahali pa kufikia.
Kuhusu hali ya ulinzi na usalama wakati wa Bunge, mkuu huyo wa mkoa alisema wamejipanga vizuri na kuwaahidi kuwa wageni wote wataondoka salama, na kwamba yeyote atakayethubutu kuchezea hali hiyo ya usalama, atachukuliwa hatua kali za kisheria kwani hawatakuwa na mchezo katika hilo.
Aidha, aliwashauri wafanyabiashara wa nyanja zote mkoani kutumia fursa hiyo ya kuingia kwa wabunge hao na wageni wao kujiongezea kipato katika biashara zao. Aliongeza kuwa kama watawahudumia vizuri watajipatia wateja katika kipindi hiki na wengine kuwa nao kwa kipindi cha miaka mitano ya uhai wa Bunge la 11.
No comments:
Post a Comment